JESHI la Polisi Mkoa wa Kinondoni, jijini Dar es Salaam,
limekiri kumshikilia kwa saa kadhaa kwa mahojiano mmiliki wa ‘blog ya
Uturn’, Mange Kimambi, kwa madai ya kumhusisha muigizaji maarufu nchini,
Vicent Kigosi au Ray, na kifo cha nguli wa tasnia hiyo, Steven Kanumba,
‘The Great’.
Akizungumza na Tanzania Daima jana, Kamanda wa Polisi mkoa huo,
Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Charles Kenyella, alisema Ray
alikwenda kulalamika kwenye kituo hicho, kuhusu maneno yaliyoandikwa
kwenye mtandao huo akiomba msaada wa jeshi hilo.
“Ninathibitisha kwamba huyo dada tulimshikilia hapa kwetu tangu jana
(juzi), tumemwachia leo (jana), kwa sababu dhamana ni haki yake, ila
tunaendelea na upelelezi, maana anadaiwa kutuma taarifa kwenye mtandao
akimhusisha Ray na kifo cha Kanumba.
“Hiyo blog haijahalalishwa kutoa taarifa za kukashifu na
kuwadhalilisha watu… ameandika skandali kwa Ray, tukiiachia hii, maneno
hayo yanaweza kuonekana halali na kuleta maafa katika jamii, hasa kwa
huyo anayetajwa,” alisema Kamanda Kenyella na kuongeza kwamba kesi iko
mahakamani, hivyo si vema kuingilia upelelezi.
Kwa upande wake, Ray aliyekuwa rafiki wa karibu wa marehemu Kanumba,
alisema kitendo hicho kinahatarisha maisha yake, hivyo ameapa
kulishughulikia suala hilo, huku akisisitiza kwamba suala hilo
linamvunjia heshima na kumharibia kazi yake.
“Hiki sio kitu cha kweli, Kanumba ni mdogo wangu na tumetoka mbali
kimaisha, huyu dada Mange Kimambi simjui… ameandika uongo, sijajua hizi
habari amezipata wapi hii ni kutaka kunishushia heshima katika jamii.
“Uigizaji ndiyo kazi yangu, kwa hiyo anapoandika na kuweka kwenye
intaneti inayosomwa dunia nzima, anataka kuniharibia kazi yangu? Anataka
kuniharibia maisha? Anataka kunipotezea mashabiki?
“…Unategemea watu wanioneje? Hili sitaliacha, nitalifanyia kazi na
kulifikisha mahakamani ili iwe fundisho kwa wanaotumia kalamu zao kutaka
kuwaharibia wengine, chochote kitakachonikuta nitadili na huyo mama...
haya ni maisha, nitaendelea kuvumilia Mungu yupo,” alisema Ray
anayetamba kwenye medani ya filamu ndani na nje ya nchi.
Juhudi za kumpata Mange, aliyewahi kuandaa shindano la urembo la Dar
Indian Ocean 2006 na kumwibua Wema Sepetu, hazikufanikiwa baada ya simu
yake kutopatikana.
SOURCE:TANZANIA DAIMA