KAJALA & CHAMBO Mumewe wa ndoa
HATIMAYE upande wa Jamhuri katika kesi ya kutakatisha fedha
haramu inayomkabili msanii wa filamu nchini, Kajala Masanja na mumewe
Faraja Chambo, jana uliwasilisha hati mpya ya mashitaka waliyoifanyia
marekebisho na kisha kuwasomea upya washitakiwa mashitaka yanayowakabili
katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam.
Hatua hiyo ya kuwasilisha hati hiyo iliyofanyiwa marekebisho,
inatokana na amri iliyotolewa na Hakimu Mkazi, Sundi Fimbo, Machi 15
mwaka huu, muda mfupi baada ya wakili huyo wa upande wa mashitaka
kuwasomea mashitaka washitakiwa hao kwa mara ya kwanza na wakili wa
utetezi, Alex Mgongolwa, kuomba mahakama hiyo iuamuru upande wa Jamhuri
ufanyie marekebisho hati hiyo, kwa sababu hati hiyo haijataja jina la
mtu aliyeuziwa nyumba na washitakiwa hao na ipo Kitalu namba ngapi, ombi
ambalo lilikubaliwa na hakimu huyo.
Wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, (TAKUKURU),
Leonard Swai, jana aliwasomea upya hati ya mashitaka, ambayo imeletwa
mahakamani hapo kwa kibali cha Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Dk.
Eliezer Feleshi, licha ya mume wa Kajala kutokuwepo mahakamani kwa
sababu yupo gerezani akikabiliwa na kesi nyingine ya utakatishaji fedha,
ambayo haina dhamana kwa mujibu wa sheria.
Swai, alidai kuwa washitakiwa hao wanakabiliwa na mashitaka yale yale
ya awali, ambayo ni matatu na jina la mtu aliyeuziwa nyumba hiyo ni
Emilian Rugalia.
Wakili huyo wa TAKUKURU, alidai, washitakiwa hao wanakabiliwa na
mashitaka matatu, kosa la kwanza ni la kula njama kinyume na kifungu
cha 34 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ya mwaka 2007, ambako
washitakiwa wote kwa pamoja, walitenda kosa hilo la kula njama la
kuhamisha umiliki wa nyumba iliyopo Kunduchi, Salasala eneo ambalo
halijapimwa jijini Dar es Salaam.
Shitaka la pili ni kwamba, Aprili 14 mwaka 2010 walihamisha isivyo
halali umiliki wa nyumba hiyo, ambayo walikuwa wakiimiliki kwenda kwa
Emilian Rugalia, ambaye ndiye walimuuzia kinyume na kifungu cha
34(2)A(3), cha Sheria ya TAKUKURU ya mwaka 2007, na shitaka la tatu ni
la kutakatisha fedha, ambalo walilitenda siku hiyo ya Aprili 14 mwaka
2010, huku wakijiua ni kinyume cha sheria hiyo.
Hata hivyo, Kajala ambaye alikuwepo peke yake mahakamani hapo, bila
mshitakiwa wa kwanza (Chambo), ambaye ni mumewe kutokuwepo mahakamani
hapo, kwa sababu yupo gerezani kwa zaidi ya mwaka mmoja, kwa sababu
anakabiliwa na kesi nyingine ya utakatishaji fedha haramu iliyofunguliwa
mahakamani hapo, ambako kwa mujibu wa sheria, kosa hilo halina dhamana,
alikana mashitaka yote matatu na akaamriwa kurudishwa rumande hadi
Aprili 4, mwaka huu, kesi hiyo itakapokuja kwa ajili ya kutajwa.
|
No comments:
Post a Comment